Mwongozo wa kutunza Sayari yetu hai
Mpango wa pamoja kati ya Vatican na Taasisi ya Mazingira ya Stockholm


Kila kitu kimeunganishwa
Laudato si’ (91)
Ni lazima kupyaisha haraka uhusiano wetu na sayari yetu hai.
Ingawa kiwango cha changamoto hii kinaweza kuonekana cha kutisha, habari njema ni kwamba majibu tayari yako mikononi,ni juu yetu tu kuyaweka katika vitendo.
Kurasa zifuatazo zinaonesha muhtasari kuhusu masuala ambayo ni moyo wa shida yetu ya sasa. Lengo ni kufahamisha, kuhamasisha matumaini, na kuchochea mjadala na vitendo.
Mwongozo huu ni tunda la ushirikiano kati ya jumuiya za kisayansi na kiroho, na kati ya Taasisi ya Mazingira ya Stockholm na Baraza la Kipapa la Kuhamasisha Maendeleo Fungamani ya Binadamu. Unaweka mambo muhimu na masuluhisho juu ya mada muhimu pamoja na ushauri wa jinsi gani jumuiya zinaweza kujibu.
Mwongozo huu umehamasishwa na Waraka wa Pili wa Papa Francisko, wa Laudato si’: kuhusu utunzaji bora wa Mazingira Nyumba yetu ya Pamoja, ambao unaochunguza migogoro yetu ya kiekolojia na mizizi yake inayotokana na utumiaji kupita kiasi na mitindo ya sasa ya maendeleo ya kiuchumi. Masuala haya ni vipaumbele kwa Papa Francisko, Kanisa Katoliki na waamini wote, jumuiya ya wanasayansi,na raia wote,tunapojibu mwito wa kulinda na kurejesha upya nyumba yetu ya pamoja.
Hali ya hewa ni nzuri kwa wote, ni ya wote na ina maana kwa wote.
Laudato si’ (23)
Tunaishi katika mgogoro wa hali ya hewa uliosababishwa na mifumo ya kiuchumi na kijamii inayoendeshwa na nishati ya mafuta. Pasipo mwitiko mpana,mabadiliko ya tabianchi yatadhoofisha hali ambayo imeturuhusu kustawi kwenye sayari yetu. Ili kukabiliana na mgogoro huu tunahitaji kufanya mabadiliko msingi wa kiuchumi na ya tabia zetu, kutoka mifumo yetu ya kila siku ya utumiaji,na kuendeleza haki kijamii. Lakini zana tunazohitaji kuchukua hatua, ziko mikononi mwetu.
Sayari yetu ilitoa hali ya hewa tulivu ambayo iliruhusu ubinadamu na asilia kustawi kwa maelfu ya miaka. Lakini tangu kuanza kwa Mapinduzi ya Viwanda katika karne ya 18, tumetoa gesi chafuzi zaidi kwenye angahewa yetu inayopasha joto la tabianchi kwa kunasa joto la jua
Gesi hizi hutolewa kwa kuchoma makaa ya mawe,mafuta na gesi kwenye nguvu ya umeme wa viwanda na usafiri,kusambaza joto na umeme katika nyumba na majengo yetu. Tuna gesi pia kupitia kilimo kikubwa na ukataji misitu.
Ukame, dhoruba na mafuriko yamekuwa tayari ni ya mara kwa mara na yenye athari kubwa. Uhaba wa chakula na maji unasababisha njaa na migogoro. Viwango vya bahari vinaongezeka: watu milioni 150 kwa sasa wanaoishi kwenye maeneo ambayo yatakuwa chini ya usawa wa bahari ifikapo katikati ya karne.
Baadhi ya bayoanuwai katika mazingira yetu kama vile miamba ya matumbawe, imeathiriwa na ongezeko la joto hadi kiwango ambacho haiwezi kurejeshwa. Na watu maskini duniani ambao wanahusika kidogo na mabadiliko ya tabianchi, hukumbwa zaidi na athari hizo, ingawa sisi wote tutaathirika.

Kwa kupitia hatua za haraka za kuondoa haraka uzalishaji wa gesi chafuzi, tunaweza kupunguza ongezeko la joto na kuzuia matokeo yake hatarishi zaidi. Mnamo mwaka 2015, karibu nchi 200 zilitia saini mkataba mjini Paris wa kupunguza joto kupanda hadi nyuzi joto 1.5,lakini hatujachukua hatua za haraka inavyopaswa. Muongo ujao utakuwa mgumu.
Mabadiliko makubwa ya kiuchumi na kijamii yanahitajika. Lazima:
Picha: Pchoui / Getty Images.
Kwa sababu viumbe vyote vimeunganishwa, kila kiumbe lazima kitunzwe kwa upendo na heshima
Laudato si’ (42)
Ukuaji wa viwanda, wingi wa matumizi na mabadiliko katika kilimo yameleta ulimwengu ulio hai katika hatua ya mgogoro. Tumesababisha na kutoweka kwa wingi wa spishi nyingi, kuanzia na mamalia hadi mimea midogo zaidi na bakteria. Wakati ni sasa wa kubadili mkondo huu na kulinda mifumo ekolojia ya wanyamapori ambayo imebaki na kufufua ile iliyoharibiwa. Mifumo ekolojia ya wanyamapori ni msingi wa maisha na ustawi wetu.
Mifumo ya ekolojia yenye afya inayosimamia tabianchi, hutoa maji safi, dawa, husafisha mazingira, huchavusha mimea na kutoa umuhimu wa maliasili. Shughuli nyingi za kukidhi mahitaji pia zinategemea moja kwa moja huduma zinazotokana na mifumo hii. Asili ni chanzo cha thamani kinachochochea sanaa na mafunzo, na cha uzoefu wa kiutamaduni na kiroho. Kadri viwanda, kilimo na uvuvi vinapofikia mbali zaidi katika mandhari mwitu kama vile misitu, ardhi na bahari, vinaharibu utajiri wa ulimwengu ulio hai.
Katika kipindi hicho, mimea na viumbe wa maji matamu wamepungua kwa 84%. Nyuki na wachavushaji wengine wamepungua sana na kutishia usambazaji wa vyakula muhimu, matunda na mbogamboga.
Bila kuchukuliwa hatua juu ya tabianchi na ukataji miti, msitu wa mvua wa Amazonia ndani ya miaka 50 ijayo unaweza kutoweka na kuwa eneo kavu na lenye vichaka. Udongo wetu huko chini ya tishio kubwa: bila bayoanuwai katika udongo, mifumo ekolojia inayounga mkono haitaweza kudumu. Mifumo yenye afya hulinda dhidi ya athari za mabadiliko ya tabianchi, kama vile joto kali na dhoruba.

Kwa hatua ya haraka ya kuhifadhi na kurejesha mifumo ekolojia tunaweza kubadilisha uharibifu wa asili. Tunahitaji kulinda na kurejesha makazi ardhini na baharini. Haki lazima ziimarishwe za ardhi, za wakazi wa ndani na wenyeji wa asili, ambao wana ujuzi wa kina na mpana kuhusu matumizi ya busara ya maliasili.
Tunahitaji kubadili jinsi tunavyozalisha na kutumia chakula. Mbinu za kilimo cha urejeshaji zinaweza kutoa mahali asilia na kusaidia kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi. Kula nyama na maziwa kidogo na kupunguza utupaji wa taka za chakula, kutapunguza shinikizo kwenye mifumo ekolojia. Na kukabiliana na mgogoro wa tabianchi utazuia upotevu zaidi wa bayoanuwai.
Picha: ARoxo / Getty Images.
Upatikanaji wa maji salama ya kunywa ni haki msingi na ya kimataifa
Laudato si’ (30)
Tuna wajibu wa kimaadili kuhakikisha kwamba kila mtu anapata maji safi na ya kutosha kukidhi mahitaji msingi ya binadamu. Hata hivyo idadi inaongezeka ya watu wanaokosa uhakika wa maji, hasa watu maskini. Tunaweza kuhakikisha upatikanaji wa maji salama ya kunywa, usafi wa mazingira kwa wote, na matumizi endelevu ya maji katika kilimo na viwanda kwa kuyachukulia maji kama rasilimali ya thamani,kuyahifadhi na kuyasimamia kwa njia ya haki na endelevu.
Idadi ya watu wanaokosa maji safi ya kunywa, kuoshea, na kumwagilia mimea inaongezeka. Wakati mwingine hali hii inatokana na upungufu wa maji,utumiaji zaidi ovyo au kuchafuliwa. Matumizi ya maji yameongezeka mara mbili ya kiwango cha ongezeko la watu katika karne iliyopita na kanda nyingi zitakosa maji ya kutosha mbeleni.
Mabadiliko ya tabianchi pia yanasababisha uhaba na ukame baadhi ya maeneo na mafuriko ya mengine.
Takriban watu bilioni 4 wanakabiliwa na upungufu mkubwa wa maji, hasa katika nchi maskini na maeneo ya vijijini. Miji inayokua kwa kasi duniani kote pia inakabiliwa na hali hii, na mara nyingi huelekeza maji matamu mbali na vijiji. Uchafuzi wa maji unaohusishwa na utumiaji wa viuatilifu na mbolea za kemikali ni tatizo kubwa, wakati utumiaji mbaya wa maji na ongezeko la joto duniani pia unatishia usambazaji
Hivi sasa watu bilioni 3.6 wanaishi bila vyoo vya usalama na bilioni 1.7 wamekosa usafi wa kimsingi wa mazingira. Hali hii inasababisha mazingira hatarishi ya kupata magonjwa ya mlipuko kama vile kipindupindu na magonjwa mengine hatarishi yatokanayo na maji.

Maji lazima yachukuliwe kama rasilimali adimu na ya thamani. Tunapaswa kuyatumia kidogo na kwa ufanisi zaidi. Elimu kuhusu uhifadhi wa maji ni muhimu kwa ajili ya kuwasaidia watu wabadili njia wanazotumia.
Mbinu za umwagiliaji zisizo faa lazima zibadilishwe, pamoja na kupunguza uchafuzi wa mito na wa maji chini ya ardhi na baharini, na kupunguza matumizi ya kupita kiasi ya mbolea za kemikali na viuatilifu katika kilimo.
Tunaweza kuokoa rasilimali kwa kuchakata tena maji ya mvua na maji taka. Tunapolinda misitu tunavilinda vyanzo vya maji na mito. Kwani ongezeko la joto duniani ni chanzo cha uhaba wa maji. Ni masuala yanayohitaji suluhisho la pamoja.
Miili yetu imeundwa na sehemu zake, tunapumua hewa yake na tunapokea uhai na burudisho kupitia maji yake
Laudato si’ (2)
Kila mwanadamu anazaliwa na haki ya hewa safi. Duniani, watu 9 kati ya 10 wanapumua hewa iliyo na viwango vya juu vya uchafuzi. Wakati huo huo, uchafuzi wa hewa huchangia ongezeko la joto duniani na hudhuru ulimwengu asilia. Na athari za mgogoro huo zinawatesa sana masikini wasiochangia uchafuzi hasa katika miji. Hatua nyingi tunazoweza kuchukua ili kupunguza uchafuzi wa hewa zitaboresha sio tu afya bali zitaleta manufaa ya tabianchi, bayoanuwai na ubora wa maisha.
Aina kuu za uchafuzi wa hewa ya nje ni ukungu na moshi au masizi. Chafuzi hizi zinatokana na uchomaji wa nishati ya mafuta, uendeshaji magari na viwanda, harakati za uzalishaji wa nishati, na uchomaji wazi wa taka katika miji inayokua kwa kasi zinachangia kwa kiasi kikubwa ongezeko la joto duniani.
Upumuaji wa chembechembe zinazozalishwa ni hatarishi kwa afya ya wote, na husababisha magonjwa ya moyo, kiharusi na saratani ya mapafu. Nchi maskini na raia wao ndiyo wako hatarini zaidi.
Karibia watu milioni 3 hupoteza maisha kila mwaka kutokana na uchafuzi wa hewa ya ndani, hasa kutokana na moshi wa makaa, kuni na wa kinyesi cha wanyama wakati wa kupika.
Wakati watu wanachoma fueli hizi kwa kupikia au kupasha joto nyumba, uchafuzi hatari huzalishwa, kama vile chembechembe ndogo na Monoksidi kaboni ambazo hudhuru afya ya washiriki wote nyumbani, hasa wanawake na watoto nyumbani. Magonjwa ya mfumo wa upumuaji, saratani na matatizo ya macho ni miongoni mwa magonjwa ya kawaida yanayotokana na uchafuzi wa hewa ya ndani.

Teknolojia zinapatikana za kupunguza hewa chafuzi inayozalishwa na viwanda, na tunahitaji kubadilisha mifumo yetu ya usafirishaji wa nishati na udhibiti wa taka. Katika miji mikubwa, usafiri bora wa umma na kutembea na kuendesha baiskeli, pamoja na kubadili na kutumia injini za umeme, zote ni mbinu zinazopunguza uchafuzi wa hewa kutoka katika magari. Ni muhimu kuhama kutoka nishati ya mafuta kwenda nishati ya jua,upepo na maji. Inawezakana kuepuka uchomaji wazi wa taka kwa kupunguza, kutenganisha na kuchakata tena. Watu wanahitaji kutumia majiko safi ya kisasa na ya bei nafuu, na nishati mbadala kwa kupasha joto na kutoa mwanga katika nyumba zao.
Picha: Philippe Marion / Getty Images.
Kuna aina nyingi za mifumo midogo midogo ya uzalishaji chakula ambayo hulisha sehemu kubwa ya watu ulimwenguni
Laudato si’ (129)
Mbinu tunazotumia za uzalishaji na utumiaji wa chakula zina uhusiano wa karibu sana na ulimwengu unaotuzunguka, pamoja na mabadiliko ya tabianchi, bayoanuwai, matumizi ya maji na uchafuzi wa mazingira. Kilimo kinazidi kutoa malighafi kwa matumizi ya viwanda na miundombinu. Kadri idadi ya watu duniani inavyoongezeka, tunahitaji kuhakikisha uwepo wa chakula kwa wote pamoja na kuilinda mifumo ekolojia ambayo ni msingi wa kilimo.
Ongezeko la mahitaji ya chakula katika kipindi cha nusu ya pili ya karne iliyopita lilisababisha mabadiliko makubwa ya kilimo duniani kote. Mfumo wa kilimo cha viwanda uliendeshwa kwa kiasi kikubwa na utumiaji wa mitambo, aina mpya za mbegu, viuatilifu na mbolea. Hapo awali, mbinu hii iliongeza mavuno kwa wingi na baadhi ya mimea, lakini kwa sasa haioneshi uendelevu.
Kilimo kikubwa kimesababisha athari kubwa na mbaya za kimazingira na kijamii. Vyakula vingi vya kipekee na aina nyingi za mimea zimepotea, pamoja na kupotea kwa uhusiano wa utamaduni wa chakula.
Njaa inaongezeka katika zaidi ya nchi 50 huku theluthi moja ya chakula ikiharibika. Kilimo kikubwa hutegemea kwa kiasi kikubwa nishati ya mafuta na mbinu hii imebadilisha misitu mikubwa ikawa mashamba ya kilimo na kuhusishwa na uzalishaji wa theluthi moja ya gesi chafuzi.
Mbinu za kilimo kikubwa humonyoa na kuharibu udongo wenye rutuba na bayoanuwai ya mazingira jirani, na hudhoofisha uwezo wa vizazi vijavyo kulima chakula. Wakulima wa ndani na Watu Asilia wanapohama, tunapoteza kwa kasi akiba ya ujuzi na maarifa waliyonayo.

Dunia yenye joto kali itadhuru uzalishaji wa mimea na mifumo ekolojia, hivyo lazima tuchukue hatua ya mabadiliko ya tabianchi. Kupunguza upotevu wa chakula kutapunguza shinikizo kwenye ardhi na maji na kulisha watu wengi zaidi. Unapochagua lishe yenye kiasi kidogo cha vyakula vitokanavyo na maziwa na nyama utapunguza uzalishaji wa gesi na shinikizo kwenye ardhi.
Utumiaji wa mbinu za kilimo ekolojia unaweza kwa muda wa miaka michache kurekebisha ardhi, iliyoharibiwa, kuipatia nafasi uoto wa asili , kulinda udongo na kufyonza kaboni. Mashamba madogo bado huzalisha wingi wa chakula duniani na bayoanuai ni muhimu kwa uzalishaji: wazalishaji wa ndani na Watu Asilia wana ujuzi wa kipekee ambao ni muhimu kwa mustakabali wa kilimo.
Ulimwengu wa matumizi ya kupindukia ni ulimwengu unaodhulumu uhai kwa namna zote
Laudato si’ (230)
Kuongezeka kwa utumiaji na mifumo ya uzalishaji viwandani huleta madhara makubwa kwa ulimwengu asili,hasa katika suala la mabadiliko ya tabianchi,uchafuzi wa mazingira,na matumizi ya hovyo bila kujali maliasili. Viwango vya sasa vya utumiaji,hasa kwa matajiri zaidi,haviwezi kuendelezwa: ni muhimu kurekebisha maadili ya kiutamaduni ili yawe na uwiano na mazoea ya mzunguko na ya urejeshaji wa uchumi.
Tangu mwaka 1970 tumekuwa tukitumia zaidi kuliko sayari inavyoweza kuhimili. Zaidi ya hayo, asilimia 80 ya rasilimali za dunia hutumiwa na asilimia 20 tu ya watu.
Mitindo ya uzalishaji na matumizi katika ulimwengu ulioendelea kiviwanda huondoa utajiri wake wa asili wa Dunia, kama vile misitu, samaki, madini na maji. Miundo ya upotevu tunayotumia ya kuzalisha na kutumia bidhaa pia inachafua sana na kudhuru afya ya binadamu na ulimwengu hai, huku zikichangia ongezeko la joto duniani.
Taka za plastiki ni ishara mbaya inayodhihirisha utumiaji kupita kiasi. Kwa sasa, zaidi ya vipande trilioni 5 vya plastiki — vipande vidogo na vikubwa na chembechembe huelea bahari zetu, na vina athari mbaya kwa spishi za baharini na kwa bayoanuwai. Chembechembe ndogo za plastiki hupatikana kwenye chakula, maji na hata kwa mishipa ya damu. Nusu ya hizi plastiki zimezalishwa ndani ya miaka 15 iliyopita na uzalishaji unakua. Kila hatua ya mzunguko wa maisha ya plastiki unaweza kudhuru afya ya binadamu, kupitia kwa chembe za plastiki na kemikali zinazotumika kuzitengeneza.

Tunahitaji kuacha mifumo ya utumiaji na utupaji na kuelekea mbinu za mizunguko zilizo ndani ya mipaka ya kiekolojia.Hii inamaanisha kutumia tena na kushirikisha nyenzo na bidhaa.
Serikali lazima zichukue hatua zaidi na kuwajibisha makampuni kuchukua hatua dhidi ya athari zitokanazo na shughuli zao na minyororo ya usambazaji. Serikali pia zinahitaji kusaidia watumiaji kufanya chaguzi endelevu, kwa mfano kupitia ushuru wenye malengo na uchapishaji wazi wa lebo kwenye bidhaa. Kaya na makampuni yanapaswa pia kuwajibika na njia za utupaji wa taka wanazozalisha. Kimsingi zaidi, lazima njia mbadala zipatikane za ukuaji wa uchumi unaozingatia Pato la Taifa ambalo ni kichocheo kikuu cha kuongeza matumizi ya bidhaa na huduma.
Mtazamo wa kweli wa kiekolojia siku zote ni mtazamo wa kijamii;lazima ujumuishe masuala ya haki
Laudato si’ (49)
Haki za kijamii na haki za binadamu zimefungamana kupitia masuala yote ya dharura ya mazingira. Wale wanaochangia kiasi kidogo kwa madhara ya mazingira ndio hupata athari mbaya zaidi. Usawa na haki pia mara nyingi ni kiini cha suluhisho. Hatuwezi kutatua ongezeko la joto duniani, kwa mfano, bila kukabiliana na maswali ya ni nani anawajibika zaidi na janga hilo. Na haki za wanawake lazima zichukue nafasi kuu: wakati wanawake wanaelimishwa na kuwezeshwa, matokeo bora ya mazingira yanaonekana.
Utumiaji kupita kiasi wa maliasili wa mataifa yaliyoendelea kiviwanda unamaanisha kwamba mataifa maskini yanalipa gharama kubwa kwa maendeleo yao. Mfano wazi ni mabadiliko ya tabianchi: nchi tajiri zinahusishwa zaidi na mabadiliko hayo, lakini maskini na waliotengwa ndiyo wanaokabiliwa na athari mbaya.
Bayoanuwai na kilimo vinafungamana na haki na usawa. Wakati kilimo kikubwa kikizidi, haki za ardhi za watu wanaosimamia kwa mda mrefu mazingira yetu tajiri ya viumbe hai — wakulima wadogo na watu wa kiasili— mara nyingi wamepuuzwa.
Athari za mabadiliko ya tabianchi, kama vile kuongezeka kwa kina cha bahari, hali mbaya sana ya hewa na kupungua kwa mazao, zitawaathiri watu maskini zaidi. Kufikia mwaka 2050, zaidi ya watu milioni 140 katika Amerika ya Kusini, Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara na Asia ya Kusini-Mashariki wanaweza kulazimika kuhama kwa sababu ya migogoro hii.
Kila mtu ana haki ya hewa safi na maji, lakini watu maskini zaidi katika miji inayokua kwa kasi mara nyingi hukosa yote mawili na wanaathiriwa zaidi na uchafuzi wa mazingira. Vijana watalazimika kuishi na matokeo ya chaguzi za leo, na wanahitaji jukumu zaidi kutoa maamuzi yao sasa.

Wakati tunapambana na kukomesha uzalishaji wa gesi chafuzi, ni lazima tukabiliane na athari za mabadiliko ya tabianchi na kujenga ustahimilivu wa jamii, hasa kwa walio hatarini zaidi. Tunaweza kurejesha na kuhifadhi mifumo ekolojia, kujenga miundombinu ya kulinda dhidi ya mawimbi ya dhoruba na kuongezeka kwa kina cha bahari, na kulima aina za mazao yanayostahimili ukame.
Kuhama uchumi wa nishati ya mafuta,lazima pia tuzingatie “mpito wa haki”, ambao unahakikisha usalama na utoaji fursa kwa wale ambao wanaweza kupata hasara kutokana na mabadiliko haya. Na kutetea kwa nguvu haki ya ekolojia ni muhimu kwa ajili ya kujenga ulimwengu thabiti na wenye usawa.
Mambo mengi lazima yabadilike
Papa Francisko, Laudato si’ (202)
Hatujajitenga na sayari tunayoshiriki pamoja na uhai wa viumbe wengine; tuna uhusiano wa karibu na hivyo tunawajibika pia kwa kuutunza uhai huu. Ukweli huu ni lazima utambuliwe ili tukabiliane na changamoto za hatua hii muhimu katika historia. Kilicho hatarini ni haki za watoto wetu za usalama wa tabianchi, maji safi na hewa, chakula cha kutosha, usalama wa kimwili, na maajabu ya sayari iliyo tajiri na uhai.
Hatuwezi kuepuka migogoro pacha ya mabadiliko ya tabianchi na upotevu wa bayoanuwai, wala kukabiliana na uchafuzi wa mazingira, uharibifu wa rasilimali, umaskini na ukosefu wa haki, bila kubadilisha tabia ya mifumo iliyopitwa na wakati, utamaduni na uchumi. Ni lazima tukomeshe uhusiano tulionao wa kuinyonya sayari na kukumbatia uhusiano unaoegemea kwenye uwakili na utunzaji. Ingawa mabadiliko kama hayo tayari yameshaanza, uzito wa hali iliyopo unahitaji hatua kubwa zaidi.
Watu na Jumuiya lazima washirikiane ili kuhakikisha kwamba wanaotoa maamuzi na kushikilia wajibu na mamlaka zaidi wanaelewa kwamba hatua zinazohusiana na masuala haya ni za kipaumbele kwa watu wanaowahudumia, na kwamba wanawajibika.
Iwapo wakati huu ni wa majaribio, ni wakati pia wa fursa: tunaweza kuunda upya uhusiano wetu na sayari sio tu kwa kujiendeleza,lakini pia kustawi na kunawiri.
Mungu mwenye nguvu zote, upo katika ulimwengu wote
na katika viumbe vyako vidogo.
Unakumbatia kwa huruma yako yote yaliyopo.
Mimina juu yetu nguvu ya upendo wako,
ili tuweze kulinda maisha na uzuri.
Utujaze amani, tupate kuishi
kama kaka na dada, tusimdhuru mtu yeyote.
Ee Mungu wa maskini,
utusaidie kuwaokoa walioachwa na kusahauliwa wa dunia hii,
wa thamani sana machoni pako.
ulete uponyaji katika maisha yetu,
ili tuulinde ulimwengu na tusiupore,
ili tupande uzuri, si uchafuzi na uharibifu.
Gusa mioyo ya wale wanaotafuta faida tu
kwa gharama ya masikini na ardhi.
Utufundishe kugundua thamani ya kila jambo,
Tujazwe na hofu na kutafakari,
kutambua kwamba tumeunganishwa kwa kina
na kila kiumbe tunaposafiri kuelekea kwenye nuru yako isiyo na mwisho.
Tunakushukuru kwa kuwa nasi kila siku.
Ututie moyo, tunaomba, katika mapambano yetu
kwa haki, upendo na amani.
Papa Francisko, Laudato si’ (246)
Taasisi ya Mazingira ya Stockholm ni Shirika la kimataifa lisilo la faida la utafiti na sera linaloshughulikia changamoto za mazingira na maendeleo.
Kitengo cha Baraza la Kipapa huwasaidia viongozi na washiriki wa Kanisa Katoliki kuhamasisha maendeleo fungamani ya binadamu na utunzaji wa nyumba yetu ya pamoja.
Katika Laudato si’, Papa Francisko anatualika kukuza “ufahamu wa upendo” wa nyumba yetu ya pamoja na kutenda kulingana na maadili tunayoyathamini. (Laudato si’, 220).
Jukwaa la Kazi ya Laudato si’ limechochewa na maono fungamani ya kiekolojia ya Laudato si’. Jukwaa hili huwezesha jumuiya, taasisi na vikundi kuwa na mabadiliko ambayo wanataka kuyaona ulimwenguni katika enzi ya sasa ya dharura ya sayari. Jifunze zaidi kuhusu yale unayoweza kufanya ili kuleta mabadiliko chanya.
Tembelea Jukwaa la Kazi la Laudato si’: laudatosiactionplatform.org
Chapisho hili liliundwa awali kama kijitabu cha kurasa 20 kilichochapishwa.



